Ijumaa, 16 Februari 2018

WAZIRI MKUU WA ETHIOPIA ATUMA WARAKA WA KUJIUZULU

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn, ametuma waraka wa kujiuzulu kufuatia wimbi la maandamano dhidi ya serikali. Habari hizo zimeripotiwa na kituo cha matangazo cha Fana. Msomi huyo aliyegeuka kuwa mwanasiasa, amekuwa akiiongoza nchi hiyo ya Afrika Mashariki tangu alipofariki dunia Waziri Mkuu wa zamani Meles Zenawi, mwaka 2012. Kituo cha matangazo cha Fana kimesema Waziri Mkuu amewasilisha waraka wa kujiuzulu bungeni na kwamba anataraji maombi yake yatakubaliwa. Ripoti ya kituo cha matangazo cha Fana imeongeza kusema Waziri Mkuu Desalegn amejitahidi awezavyo kuupatia ufumbuzi mzozo unaoikumba nchi hiyo na kwamba kujiuzulu kwake ni sehemu ya ufumbuzi huo. Waziri Mkuu Hailemariam Desalegn ataendelea na wadhifa huo hadi serikali ya mpito itakapoundwa. Ethiopia inagubikwa na wimbi la malalamiko tangu miezi kadhaa iliyopita ambapo waandamanaji wanadai uhuru zaidi. Mnamo siku za hivi karibuni serikali ya mjini Addis Ababa imewaachia huru mamia ya wafungwa, wakiwemo wa kisiasa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni