Jumatatu, 12 Machi 2018

PIERRE NKURUNZIZA APEWA CHEO NA CHAMA TAWALA

Chama tawala nchini Burundi kimempa cheo cha ''mlinzi aliyetukuka'' rais Pierre Nkurunziza wakati ambapo wakosoaji wake wanadai kwamba anataka kubakia madarakani milele. Katibu Mkuu wa chama tawala cha CNDD-FDD Evariste Ndayishimiye amesema kupitia njia ya vidio katika mkanda uliotumwa kwa shirika la habari la AFP na kuthibitishwa na afisa mmoja, kwamba rais Nkurunziza ni mzee wao,baba yao na mshauri wao. Wakosoaji wamelalamikia kilichotokea wakisema kwamba ni kumpa umaarufu wa kuonekana kuwa ni Mfalme Nkurunziza. Kwa sasa kura ya maoni kuhusu Katiba iliyopangwa kufanyika mwezi Mei mwaka huu huenda ikampa nafasi ya kugombea tena katika uchaguzi wa mwaka 2020 na kumfungulia njia ya kubakia madarakani hadi mwaka 2034.

Jumatano, 7 Machi 2018

TAARIFA KUTOKA TFDA

Mamlaka ya chakula na dawa nchini TFDA imesema Tanzania itajiunga na mataifa mengine kuzuia uingizaji wa Soseji kutoka Afrika Kusini zilizobainika kuwa na bakteria aina ya Listeria, iliyosababisha vifo vya watu takriban 180 nchini Afrika Kusini tangu 2017. Tayari Kenya, Zambia, Malawi, Botswana, Zimbabwe, Swaziland na Msumbiji zimepiga marufuku bidhaa za nyama ya kusindika kuingia nchini mwao. Bakteria ya Listeria inasemekana kusababisha homa kali, kuharisha na pia kuwa na athari katika mfumo wa damu.